NATAKA BIASHARA INAYOLIPA NIWAJENGEE WAZAZI WANGU NYUMBA, NILIYO NAYO HAILIPI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NATAKA BIASHARA INAYOLIPA NIWAJENGEE WAZAZI WANGU NYUMBA, NILIYO NAYO HAILIPI


Kwenye kipengele hiki cha Ongea na mshauri wako leo hii tutajibu swali la msomaji wa blogu hii mwanadada(mama) kutoka kule mkoani Kigoma na kama ilivyokuwa ada, swali lake nitaliweka hapa mezani pasipo kuongeza wala kupunguza nukta hata moja na pia siwezi kutaja jina lake kwani hakuniruhusu kulitaja hapa. Ujumbe wake alionitumia kupitia text meseji ulisomeka kama ifuatavyo;

Asante kwa majibu mazuri kwa ndugu yetu anayetamani kuwa BILIONEA!  But hata mm natamani .kaka naomba msaada kwa haya machache nitakayouliza pia ushauri nini nifanye?  Umri wangu miaka  29, mwaka 2014 nilianza lasimi kazi ya kusaka pesa, baadae ya kukaa nyumbani miaka 4 kama mama Wa nyumbani nikihudumia familia yangu, Mume wangu alinipa laki 9 akanishauri nifungue duka la chakula, nikafanya hivyo lakin sehemu alionichagulia mwenzangu haukuwa sahihi kwa duka LA chakula kwan mauzo yalikua chini sana,cku nyingine nilikua nauza hadi sh200/1000 ,hapo unatumia nauli,ushuru na pango ya soko. Baadae ya mwaka nilifunga duka nikarudi kuhudumia familia, baadae nikajifunza mambo ya ujasiriamali nikawa natengeneza vitu vyangu na kuuza (Batiki & sabuni unga na za Maji). Ujuzi mkononi, nikawa Fundi mzur sana, shida moja kwangu ikawa in soko huku  kwetu Kigoma, Mungu ameendelea kunitumia nikajifunza tena  kupka ubuyu Wa Zanzibar na Karanga za mayai, Mungu ni mwema nimeanza kupata wateja wazr. Naomba msaada kwa hili Wazo langu. Nimekaa nikawaza  je nitawajengea lin wazazi wangu maana hizi Biashara haznilipi sana? Mungu akanipa Wazo nikalifanyia uchunguzi nikaona ni bora,  nikafanya survey nikaona hicho kitu kwa hapa Kigoma anaetengeneza wote wanaouza wanatoa  Dar, walifurahi sana kwa kupata bidhaa karbu na makaz yao, nikawa nimeandika business plan yangu vzr tu ikawa na mtaji Wa million 2, toka mwezi Wa 3 mwaka huu, nikamwonesha mume akaipenda. Shida yangu ni kwamba nimekosa hiyo pesa ili nifungue mradi wangu ambao hata nikikopa baada ya mwezi 1 narudisha hiyo pesa tena yote nabaki na faida yangu. Nimejtahidi sana kumshawishi Mume wangu amesema niendelee kwanza na Biashara hiz ndogondogo. Nifanyeje ili ndoto zangu zitimie ktk hili ikiwa na solo liko waz?

MAJIBU.
Kwanza kabisa niseme kwamba swali lako limenifurahisha na kunigusa kwani umetaja kuhusiana na azma yako ya kuwajengea wazazi wako nyumba. Nadhani Duniani hakuna mtu hata mmoja ambaye katika ndoto zake hajawahi kufikiria kuwafanyia wazazi wake jambo fulani kama fadhila, na cha kufurahisha zaidi wewe ni mwanamke tena ambaye umeolewa lakini bado katika nafsi yako una shauku ya kuhakikisha unawafanyia wazazi wako jambo kabla muda haujazidi kuyeyoma. Unawakilisha karibu kila binadamu aliyezaliwa na wazazi hapa duniani. Zipo baadhi ya jamii au makabila ambayo mwanamke akishaolewa kuwajengea wazazi wake ama kuwafanyia jambo kubwa kama fadhila ni mwiko.

Kasumba hii ni mbaya haifai kabisa na inafaa itupiliwe mbali, mwanamke kama ana nafasi kiuchumi ana haki ya kuwafanyia wazazi wake jambo lolote zuri bila kujali ameolewa ama hajaolewa. Kwahiyo nakupongeza sana dada kwa mawazo yako mazuri, big up!


Kama sijakosea, umetaka ushauri juu ya wazo lako jipya la biashara ambalo kulingana na utafiti wako wa awali(survey) umebaini kwamba biashara hiyo inao uwezo mkubwa wa kuleta faida na hata kama ungefanikiwa kupata mkopo mahali ungeweza kuurejesha mkopo huo ndani ya kipindi kifupi sana huku ukibaki na mtaji uliokopa kama faida.

Kulingana na maelezo yako inaonekana wazi kwamba tatizo lako kubwa ni mtaji mdogo na mumeo ambaye angeweza kukuongezea mtaji huo tayari keshaonyesha kutokufanya hivyo kutokana na sababu kwamba mtaji aliowahi kukupa mara ya kwanza wa kufungua duka la vyakula la rejareja haukuweza kuzaa matunda yeyote yale ya maana.


Mimi wazo lako hili jipya la bishara sina tatizo nalo hata kidogo kwamba lina uwezo wa kulipa, inawezekana kabisa kweli likawa ni zuri na litakalolipa lakini ukumbuke pia kwamba karibu kila mtu anayeanzisha biashara yake mpya mwanzoni huona kabisa akilini kwamba biashara iliyoko mbele yake itamlipa na utafiti humuonyesha hivyo. Lakini atakapoingia ‘field’ uwanjani, uzoefu huonyesha kuwa  wengi hukutana na changamoto nyingi, hali tofauti au kukuta mambo ni kinyume kabisa na vile utafiti ulivyoonyesha awali. Sababu zaweza kuwa nyingi lakini kubwa zaidi hutokana na ufinyu wa mtaji, ushindani mkali, ukosefu wa maarifa sahihi juu ya biashara husika au uzoefu na usimamizi usio makini.

Ushuri wangu mimi kwako hautakuwa tofauti sana na ule aliokupa mumeo wa kuendelea kuwa na subira kwanza huku ukiendelea kwanza kufanya hizo biashara ndogondogo za batiki, sabuni za unga & za maji, karanga za mayai na ubuyu wa Zanzibar, biashara ambazo wewe unasema hazilipi au faida yake ni kidogo sana. Nasema hivyo dada angu kwani nijuavyo mimi siku zote mtaji wa kukopa ni hatari sana kuutumbukiza kwenye biashara mpya unayoianza na ambayo bado hukuwa na uzoefu nayo angalao wa miezi kadhaa, au ungelikuwa tayari unao mtaji wako mwenyewe mkononi unaokwenda kuanza nao.


Ni afadhali pia hata kama ungelikuwa na kiasi fulani cha mtaji huo kama nusu yake au robotatu ningekushauri uanze tu any way, lakini midhali mtaji hauna kabisa unategemea kuazima mahali au ni kidogo mno ni bora kabisa ukaendelea kudunduliza kidogokidogo kutoka kwenye biashara ulizozizoea tayari na ulizo na uhakika nazo mpaka angalao utakapoweza kupata nusu ya mtaji unaohitaji ndipo ufikirie kutafuta kiasi kilichobakia mahali pengine.

Vinginevyo basi ningekushauri pia ikiwa huwezi kabisa kujizuia kuianza ukihofia fursa hiyo kupita muda wake au kunyakuliwa na watu wengine, basi ianze tu hivyohivyo kwa mtaji uliokuwa nao mwenyewe hata ikiwa ni mdogo kiasi gani mpaka mtaji wako utakapotengemaa pasipo kwanza kukopa mhali popote. Lakini angalizo hapa ni kwamba lazima upime kwanza kwani  zipo biashara asili yake unaweza ukaanzia chini kabisa kimtaji na nyingine ambazo asili yake ni lazima uwe na mtaji kiasi kilekile kinachohitajika ndipo ziwezekane kuanza.


Mawazo kwamba ukikopa baada ya mwezi mmoja tu tayari utakuwa umesharejesha mkopo wa watu yaache kwanza kwani yamewahi kuwapotosha watu wengi hatimaye wakajikuta wametumbukia katika shimo refu la madeni wasiloweza kujinasua kirahisi. Ndoto zako zitatimia tu suala hili ukiliwekea subira, usikurupuke, ni kweli muda unapita na fursa hazisubiri lakini wakati mwingine kulazimisha mambo kwaweza kufanya hali kuzidi kuwa mbaya.

Mumeo tayari keshaonyesha ni mtu anayependa maendeleo na ndiyo maana mwanzoni alikubali kukupa mtaji wa duka. Angekuwa hakutakii mema sidhani kama hata angekuruhusu ufanye hizo biashara ndogondogo, tena ameendelea kukutia moyo uwe na subira kwanza ukizifanya kabla hajakuongezea mtaji wa hiyo biashara inayolipa.


Usije ukafikiria namtetea kwa vile ni mwanaume kama mimi hapana, yeye pia amepima na kuiona hatari kubwa inayoweza kuambatana na maamuzi ya haraka ya kutumbukiza mtaji wa kukopa katika biashara mpya isiyopata bado uzoefu wa kutosha. Nielewe vizuri sana hapa, si kwamba tatizo lipo kwenye uzoefu hapana kwani uzoefu watu huweza kuupata mbele ya safari, tatizo kubwa hapa ni MTAJI WA KUKOPA, ikitokea umezama utaurudisha kwa nji gani?

Hebu jikomaze kwanza kidogo uwe na uwezo angalao wa mtaji kiasi nusu au robotatu wa hiyo biashara halafu kile kiasi kitakachobakia shemeji naamini kabisa atakuwa tayari kukuongezea bila shaka yeyote. Kumbuka ile ni biashara na haipaswi kuingilia mahusiano yenu kwa namna yeyote kama mke na mume. Ndoa nyingi zimevurugika kisa masuala haya haya ya kichumi na biashara.


Mumeo anaweza akakupa fedha na kwa bahati mbaya kama ilivyotokea mwanzoni mtaji ukajakukata tena, huoni anaweza akahisi pengine fedha kuna mahali unazipeleka, akaishia hata kuhisi labda unacho ‘kidumu’(mwanaume wa pembeni) mahali kinachotafuna pesa zako na huo ndio ukaanza kuwa mwisho wa ndoa yako?

Huo ndio mwisho wa majibu ya swali letu la leo kutoka kwa mwanadada wa kule Kigoma, mpenzi msomaji tunakaribisha maswali na changamoto mbalimbali kwenye biashara ndogondogo, hatutozi chochote kwa maswali mafupimafupi kama haya na huwa tunajibu kupitia meseji, wasap na email lakini wakati mwingine majibu tunayaweka hapa kwa manufaa ya wasomaji wengine. ASANTE SANA.

………………………………………………...........

Darasa letu la whatsapp bado linaendelea kila siku na kuanzia mwezi huu wa 7,nusu ya pili ya mwaka tutahakikisha mazimio tuliyojiwekea Januari yanakamilika hivyo kama ulikuwa hujajiunga bado hujachelewa. Kiingilio ni shilingi elfu 10 tu, unapata vitabu, masomo mbalimbali ya semina zilizopita, michanganuo ya kuku aina zote nk. pamoja na fursa ya kuendelea kupokea masomo mazuri kila siku na kuungana na group la watu makini katika biashara zao mbalimbali. Wasiliana nasi kupitia SIMU: 0712202244 au WHATSAP: 0765553030

Vitabu pia vipo tazama hapa chini au unaweza kutembelea, SMARTBOOKS TANZANIA kwa maelezo zaidi.








0 Response to "NATAKA BIASHARA INAYOLIPA NIWAJENGEE WAZAZI WANGU NYUMBA, NILIYO NAYO HAILIPI"

Post a Comment