MIFEREJI YA KIPATO NI KWA WALIOFANIKIWA, KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NI KUPOTEZA MUDA, NGUVU NA MALENGO BURE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MIFEREJI YA KIPATO NI KWA WALIOFANIKIWA, KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NI KUPOTEZA MUDA, NGUVU NA MALENGO BURE

Tunapozungumzia biashara kubwa na biashara ndogo ndogo kuna tofauti kubwa sana. Hali kadhalika  unapotaja mfanyabishara mkubwa na mdogo ni watu wawili tofauti kabisa. Ushauri unaoweza kumpatia mfanyabiashara mkubwa siyo ushauri unaoweza kumpa mfanyabiashara mdogo ingawa kuna badhi ya mambo mengine yanayoweza kuwafaa wote wawili..

Vile vile mtu nayefanya kazi(mwajiriwa) na yule aliyejiajiri mwenyewe kupitia biashara ni watu wawili tofauti kabisa na ujumbe au ushauri unaoweza kumpatia mmoja kati ya hao huwezi ukautumia ujumbe huohuo kumpatia mwenzake, hautaweza kumsaidia. Nasema hivi kwasababu sisi tunaoandika makala hizi za ujasiriamali kuwaelimisha watu mbalimbali, huwa wakati mwingine tunafanya makosa pale tunapodhani kwamba wasomaji wetu au hadhira inayotufuatilia ina mahitaji yanayofanana.


Mfano niliwahi kuandika makala moja katika group la whatsapp isemayo, “KUKOPESHA SIYO KWA AJILI YA BIASHARA NDOGO NDOGO BALI BIASHARA KUBWA” nikiwa namaanisha kwamba biashara ndogo inapojiendesha kwa kukopesha wateja huwa haikawii kufa kutokana na mzunguko wake wa pesa kuwa mdogo, lakini kwa biashara kubwakubwa kukopesha wateja ndiyo tabia yake kubwa na watu huweza kukaa na deni hata mwezi, miezi miwili nk. ndipo huja kulipa.

Katika kitabu pia nilichoandika kiitwacho, MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA, nilieleza kwamba Mifereji ya pesa ni kile kipato mtu unachopata nje ya shughuli zako za msingi. Shughuli ya msingi hapa ni kama vile ajira au biashara uliyokuwa umeshaianzisha siku nyingi na inakuletea tayari mapato. Kwa hiyo huwezi ukasema unaanzisha mfereji wa pesa wakati huna bado shughuli iliyokwishaanza kuonyesha mafanikio, hapa ndipo unapata pointi yangu kwamba, “Mifereji ya pesa ni kwa ajili ya wale waliofanikiwa na wajasiriamali wadogo kabisa ambao ndio wanaanza wanapoteza muda wao bure kujaribu kuanzisha mifereji mingi ya kipato”, nilikuwa namaana hiyo.


Pia ukurasa wa pili wa kitabu hicho nikaaandika tena hivi, “Watu matajiri kanuni hii wao huitumia vizuri zaidi na huwa inawasaidia kuliko masikini, hebu fikiria ni tajiri gani chini ya jua anayemiliki kamradi kamoja?” Ikiwa hauna biashara ya msingi au kazi ambayo tayari inakuingizia kipato, wewe mifereji ya kipato siyo ya kuhangaika nayo itakupotezea muda, nguvu na malengo yako bure, ni bora ukatafuta kwanza kazi au biashara moja, ukaweka nguvu zako zote pale mpaka itakapoanza kuleta mafanikio ndipo ufikirie kuanzisha kitu kingine.

Ninachotaka uelewe hapa ndugu msomaji  siyo kingine bali, “UMUHIMU WA LENGO(FOCUS) KATIKA KUFANIKISHA KWANZA JAMBO LOLOTE LILE KWA UFANISI MKUBWA KABLA HUJAHANGAIKA NA MAMBO MENGINE YANAYOWEZA KUKUTOA KWENYE LENGO LAKO KUU
Ndio maana pale mwanzoni nikaanza kwa kusema kwamba, siyo kila mtu atahitaji ushauri unaofanana na wa mwenzake na biashara inapokuwa bado ni ndogo inahitaji mtu kuwa na malengo machache  utakayoweza kuyafanyia kazi barabara kuliko kuwa na utitiri wa malengo(vipaumbele vingi) ambayo hatimaye vitakufanya utawanye nguvu na rasilimali chache ulizokuwa nazo na kisha kushindwa kufanikisha hata lengo moja kati ya hayo mengi.


Bila shaka unaona matajiri au watu waliofanikiwa kimaisha wakiwa na miradi mingi(Mifereji ya pesa). Usifikiri eti walipoanza walikuwa hivyo hapana, walielekeza kwanza nguvu katika mradi au shughuli moja tu mpaka walipohakikisha imezaa matunda yanayoonekana ndipo sasa wakaanzisha mifereji mingine ya kuwaingizia kipato. Watu wengi wanaoanza biashara hufanya sana kosa hili la kudhani kwamba wanaweza wakaanzisha mifereji ya kipato kabla biashara ya msingi haijatengemaa vya kutosha.

Hali ndivyo ilivyo pia kwa wale walioajiriwa , kama unafanya kazi mahali inakubidi unapoanzisha mfereji wako wa kipato basi(biashara ya pembeni) basi uhakikishe unachukua tahadhari kubwa sana, muda wa kuifanya biashara hiyo usije ukaingiliana na muda wako wa kazi ya msingi kwani utajikuta napo unatawanya nguvu kama tulivyoona kwenye biashara na matokeo yake ni kuharibika kwa vyote viwili, kazi na mfereji ulioanzisha.


Kumbuka unahitaji  nguvu nyingi sana na shabaha ili uweze kufanikiwa katika jambo moja, unadhani basi utaweza kufanikiwa kirahisi katika mambo mengi kwa nguvu hiyohiyo moja uliyokuwa nayo?

Watu wengi hulalamika na kusema kuwa kanuni ya mifereji ya pesa haitekelezeki kirahisi, lakini huwa nawaambia kwamba kanuni hii ili iweze kutekelezeka vizuri mtu unapaswa kwanza uwe tayari una kazi/biashara inayokuingizia fedha zitakazokuwezesha kusapoti hiyo mifereji mipya itakayoanzishwa pamoja na kukuwezesha wewe menyewe kuishi vinginevyo ukiwa unafikiria leo utakula nini hata mawazo ya hiyo mifereji yenyewe ya pesa sijui kama yataibuka akilini.

HITIMISHO
Elekeza kwanza nguvu zako zote na malengo kwenye eneo au shughuli ile inayokupatia fedha, acha mambo mengine yote mpaka uhakikishe kwanza umefanikiwa katika eneo/kazi/biashara hiyo ndipo ufikirie kuanzisha vitegauchumi vingine. Kufanikiwa hapa simaanishi mafanikio makubwa sana hapana, bali ule uwezo wa kuendesha hiyo mifereji mingine kwa kutumia mapato ya hiyo shughuli yako ya msingi.

………………………………………………
Mpenzi msomaji wa makala hizi nachukua fursa hii kukujulisha kwamba mwanzoni mwa mwaka huu tuliahidi katika group la michanganuo, MICHANGANUO ONLINE kwamba tutakuwa na michanganuo bunifu 12 sawa na miezi yote 12 ya mwaka 2018.
Mpaka sasa hivi michanganuo tuliyojadili katika group ni 3 tu. Kuelekea nusu ya mwaka uliobakia miezi mingine 6 tumebadilisha mikakati kidogo, badala ya kuwa na masomo ya kila siku ya mzunguko wa fedha, tuta ‘focus’ zaidi katika hiyo michanganuo 9 iliyobakia. Hivyo tutakuwa na semina(siyo kila siku) zitakazohusu namna ya kuandika michanganuo hiyo bunifu hatua kwa hatua kwa kina kabisa.

Dhamira yetu na malengo tuliyoanza nayo January vipo palepale wala hakuna kilichotetereka kwani makala za FEDHA(Mtiririko wa pesa) badala yake tutazihamishia hapa katika blogu ya jifunzeujsiriamali kila siku. Ila Masomo yaliyokwishapita ambayo sasa yamefikia vitabu 2 tutaendelea kuwapa free washiriki wapya wanaojiunga na group hilo. Ikiwa hujajiunga bado na group jiunge sasa ni sh. Elfu 10 tu, kwani semina zilizobakia hatutaziweka katika vitabu tena, ikipita imepita. Pia bei ya kujiunga na group kwa washiriki wapya itapanda kuanzia mwezi wa 9 na kuwa sh. Elfu 20.

JIANDAE KWA MCHANGANUO WA BIASHARA BUNIFU INAYOLIPA MWEZI HUU WA JULY, NDANI YA GROUP LA WATSAP LA MICHANGANUO-ONLINE

Peter Augustino.

0 Response to "MIFEREJI YA KIPATO NI KWA WALIOFANIKIWA, KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NI KUPOTEZA MUDA, NGUVU NA MALENGO BURE"

Post a Comment