KITABU SIRI YA MAFANIKIO YA MAISHA YA DR. REGINALD MENGI: NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KITABU SIRI YA MAFANIKIO YA MAISHA YA DR. REGINALD MENGI: NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA


I CAN, I MUST, I WILL-THE SPIRIT OF SUCCESS. Binafsi nimefurahishwa sana na kuzidi kuhamasika kutokana na kitenndo cha Mhamasishaji wangu mkubwa tangu nikiwa mtoto Dokta Reginald Abraham Mengi kuandika kitabu kinachohusu jinsi alivyofanikiwa kimaisha na historia ya maisha yake tokea akiwa mtoto mdogo akichunga mbuzi kijijini kwake kule Machame. Kitendo alichokifanya Mzee Mengi kwa kweli hufanywa na watu matajiri wachache sana hasa katika nchi zetu za Kiafrika.

Kwa kipindi kifupi ambacho nimekuwa nikiandika na kuuza vitabu vya ujasiriamali hususani vile vinavyohusiana na maendeleo binafsi ya watu kama kina Reginald Mengi kwa lengo la kuhamasisha umma uweze kuiga mifano ya watu hao katika kujiondoa kwenye lindi la umasikini wa kutisha, nimekutana na vikwazo kdhaa na kimojwapo ni baadhi ya watu au wateja wa vitabu hivyo kuwa wazito kuvinunua kwa madai kwamba wangependelea zaidi vitabu vilivyoandikwa moja kwa moja na watu hao waliofanikiwa na wala siyo kwa kupitia waandishi wa vitabu au waandishi wa habari.

Kitendo cha Mzee Mengi ni jawabu maridhawa kwa kundi hili la wateja na kwa kweli ingelikuwa ni jambo zuri kama angalao kila mtu ambaye anatazamwa kwenye jamii kama kioo na kundi kubwa la watu basi akaandika historia ya maisha yake au hata kitabu chochote kile ambacho kitaondoa kiu ya wale ambao wangependa kusoma kazi zao moja kwa moja kutoka kwao. Ni kweli kabisa hata mimi natamani sana kusoma kitabu hicho hata ikiwa historia ya Mzee Mengi naifahamu, huwezi kujua kila kitu, kuna vitu ambavyo akiviandika mtu mwenyewe ndipo unapoweza kupata uhalisia wa mambo.


Mzee Mengi amewataja watu mbalimbali wengi waliomhamasisha katika safari yake hii ya mafanikio akiwemo Mzee Alli Hassan Mwinyi(Mzee Ruksa) na wengineo wengi, metoa pia mfano mwingine wa kuigwa kuwa ni Rais wa sasa Dr. John Pombe Magufuli kuwa ana ile roho ya kijasiriamali ya kusema “NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA”.

Hakuna kinachoshindikana mtu ukijiamini, Dr. Mengi siri yake kubwa aliamini kwamba anaweza hata pale ambapo kulijitokeza watu waliomkatisha tamaa. Wakatishaji tamaa hata leo wapo na wataendelea kuwepo siku zote hivyo kikubwa ni kuiga roho hii anayotufunza Mzee Reginald Mengi katika kitabu chake hiki cha I CAN, I MUST, I WILL-THE SPIRIT OF SUCCESS(NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA)


Katika kitabu hiki bila shaka, ijapokuwa bado sijakisoma rasmi lakini ni lazima nikisome, Mheshimiwa Mengi atakuwa hajaacha kugusia kuhusiana na suala zima la kiafya kwani bila afya njema hata utajiri na mafanikio sio kitu tena, nimefurahi alivyoelezea kilichomsukuma aandike kitabu hiki kuwa ni  pamoja na wosia wa mwanaye kipenzi, Rodney ambaye kwa sasa ni marehemu aliyemsisitizia sana juu ya kufanya mazoezi ya viungo kila siku. Mwanaye huyu alikuwa mtu makini sana kwani alifahamu fika hatari za kiafya zinazoweza kumpata mtu mwenye uwezo kama baba yake na hata wale watu wa kawaida yakiwemo magonjwa mengi yasiyoambukiza kama magojwa ya moyo, unene kupita kiasi na mengineyo.



0 Response to "KITABU SIRI YA MAFANIKIO YA MAISHA YA DR. REGINALD MENGI: NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA"

Post a Comment