NJIA WAJANJA WANAYOITUMIA KUPATA MATOKEO BORA ZAIDI KWA KILA WANACHOKIFANYA MAISHANI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA WAJANJA WANAYOITUMIA KUPATA MATOKEO BORA ZAIDI KWA KILA WANACHOKIFANYA MAISHANI


FANYA KILE UNACHOKIPENDA ZIDI KWA MATOKEO BORA
Kila mara huwa tunajiuliza swali hili kichwani, “ Nitatumia mbinu zipi ili kufanya matokeo ya kile ninachokifanya kuwa bora na chenye tija zaidi kuliko vile nilivyozoea kufanya?” Na hata ikiwa pengine hujawahi kujiuliza swali hilo, ni wakati muafaka sasa wa kujiuliza swali hili muhimu sana maishani. Ili kuweza kupata majibu ya swali hilo unapaswa kwanza kujibu maswali haya mengine mawili madogo yanayofuata hapa chini;

1.  Je, unaelekeza nguvu zako katika mambo sahihi?
2.  Unazijua nguvu zako ziliko au umezitawanya katika maeneo tofauti?

Tangu ulipokuwa mtoto mdogo bila shaka utakuwa umewahi kusikia ama kujifunza  medhali(msemo) huu kutoka kwa wazazi, walezi au hata kutoka kwa waalimu wako wa lugha ya Kiswahili kwamba;  Usikimbie na kuku wengi, utaambulia manyoya” Msemo huu kama ulivyokuwa na maana miaka hiyo iliyopita mpaka leo na hata kesho haitakaa ipoteze maana yake, itabakia kuwa vilevile kwamba; kulenga mambo mengi mno kwa wakati mmoja hakuwezi kutusaidia kupata matokeo bora kabisa maishani.


Haitoshi tu kudai unafanyia kazi mambo machache, lakini pia mambo hayo machache ni sahihi kwako? Hapa ndipo linapoingia suala la nguvu au uwezo uliokuwa nao. Ni kitu gani ambacho ukikifanya basi unasema, “ Ndiyo nimefanya” Kile kitu unachokiweza zaidi kushinda vitu vingine. Kufanya kitu cha namna hiyo ni lazima matokeo yake yawe ni ya kushangaza(Great!)

Moja ya siri kubwa zaidi ya mtu kuishi maisha yaliyojaa furaha ni kitendo cha kufanya shughuli au kile kitu akipendacho maishani, iwe ni kazi, biashara, au shughuli nyingine yeyote ile inayomuwezesha kuishi.


Mtaalamu mmoja katika kanuni yake ya 80/20 aliyoiita Pareto anasisitiza juu ya umuhimu wa kuelekeza nguvu katika yale mambo machache yanayotupatia tija kubwa zaidi na kuachana ama kuyapunguza yale mambo au shughuli zisizokuwa na faida ya maana. 

Mtaalamu huyo anataja mfano wa watu wa mauzo (salespeople) ambao anasema huitumia vizuri sana kanuni hiyo ya 80/20 kwa kulenga zaidi katika asilimia 20% ya wateja wao wanaowapatia mapato asilimia 80% na kutokujisumbua kabisa au kupoteza muda mwingi na wale wateja asilimia 80% ambao mchango wa mapato yao kwao ni mdogo sana.


Wajasiriamali wajanja mara zote hutambua na kuweka juhudi katika yale mambo machache tu yanayowapa matokeo yaliyokuwa bora kabisa hasa ikiwa mjasiriamali bado yupo katika hatua zake za mwanzo na rasilimali alizokuwa nazo ni chache. Kwa wajasiriamali wakubwa au wafanyabiashara ambao tayari wameshakuwa na mitaji ya uhakika wanaweza wakaamua kulenga mambo mengi kwa wakati mmoja na wakafanikiwa kwani tayari wanao uwezo wa kutumia nyenzo au rasilimali mbalimbali kutekeleza majukumu ya biashara zao.


0 Response to "NJIA WAJANJA WANAYOITUMIA KUPATA MATOKEO BORA ZAIDI KWA KILA WANACHOKIFANYA MAISHANI"

Post a Comment