HIVI UNAJUA NI NANI ANAYEDHIBITI MAISHA YAKO? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HIVI UNAJUA NI NANI ANAYEDHIBITI MAISHA YAKO?

UHURU WA KUCHAGUA UNACHOKITAKA
Kama haupo huru ni vigumu sana kupata mafanikio ya kweli katika nyanja yeyote ile ya kimaisha. Hebu Jichunguze kwa umakini kama wewe ni mtu mzima 'over 18' na bado asilimia kubwa ya mambo yako muhimu ya kimaisha huwezi kuyaamulia bila ya ushawishi kutoka kwa mtu mwingine.

Je, ni mwenza, ni ndugu yako, ni mzazi, ni mwenye nyumba, ni rafiki, ni jirani yako, ni mlezi wako, ni tajiri yako, au ni bosi wako kazini anayeyadhibiti maisha yako?

Kwa kuwa hatma ya mtu yeyote yule ipo mikononi mwake mwenyewe, haipaswi  mtu mwingine ayadhibiti maisha yako kwa namna yeyote ile. Inawezekana kwa sababu fulani mfano wa hali za kiuchumi zikamfanya mtu maisha yake yakadhibitiwa kwa muda fulani lakini hali hiyo kamwe haipaswi kuachwa na mhusika ikadumu milele kwa maisha yake yote. Ni lazima utafute mbinu za kujinasua.


Unakumbuka namna nchi hasa za Kiafrika zilivyojikomboa kutokana na ukoloni?. Basi na kwa mtu mmojammoja inafaa pia kuwa hivyo. Ni swala la muda tu binadamu kamwe hajaumbwa kudhibitiwa kama mnyama afugwaye. Hapa ninayo mifano halisi miwili ambayo mwenyewe binafsi niliwahi kuishuhudia. Kabla hatukwenda kuangalia ni nini cha kufanya ikiwa unajikuta katika hali mbayo hauna uwezo kamili wa kuyasimamia maisha yako mwenyewe tuone kwanza mifano hiyo.

Dada mmoja, hapa nitampa jina lisilokuwa la kwake kama ‘Mariam’, alikuwa akifanya kazi katika duka la tajiri mmoja. Pale dukani palikuwa na mfanyakazi mwenzake mwingine yeye nitamuita ‘Angela’. Wote wawili walikuwa wamekabidhiwa duka lile waliendeshe huku tajiri akiwa anafika pale siku za manunuzi ya bidhaa na kufanya hesabu tu. Ikafika kipindi fulani Mariam akawa anasumbuliwa na homa mara kwa mara kiasi ambacho kila mtu aliyemfahamu akawa anashituka kwa jinsi alivyokuwa akikonda siku hadi siku. Mariam alikonda hadi akafanana na mtoto mdogo.

Hata rafiki wa kiume, ‘boy friend’ wa Mariam alianza kuingiwa na wasiwasi kwani kila mtu maeneo yale kwa wale wa rika lake walianza kumtania na kumwambia, “kulikoni shemeji siku hizi mbona anakonda vile, au tayari keshaukwaa?, wahini hospitali mkapime”. Mariam alikosa kabisa raha kwani kila mtu alianza kumnyanyapaa utadhani tayari walishampima na kutambua hali yake kiafya. Na mtu aliyeongoza unyanyapaa huo alikuwa ni yule yule mfanyakazi mwenzake, Angela.

Angela alimkazania sana Mariam eti, aende kituo cha afya kujua hali yake ikiwa kama alikuwa tayari ameshaathirika na maambukizi ya vvu. Kwa kuwa kiumri Mariam alikuwa mdogo kwa Angela basi kwa kiasi kikubwa kila aliloambiwa na Angela alikubali, “ndiyo dada” japo wakati mwingine alikubali tu  kwa shingo upande.

Ilionekana Mariam anatokea familia duni na Angela kwa mbwembwe nyingi aliitisha mchango pale kijiweni, (kumbuka palikuwa ni maeneo ya biashara palipokuwa na biashara nyingi) akidai ni mchango wa matibabu ya Mariam, tumchangie kabla hajafa kwani akishakufa kuchanga ni unafiki.


Zilipatikana fedha kidogo na kwa msaada wa bosi wao zikatimia kiasi kama shilingi elfu hamsini hivi. Kwa kiasi Angela alivyokuwa akishadidia suala lile la ugonjwa wa Mariamu, mtu yeyote yule angedhani labda walikuwa ni mtu na dada yake wa damu kumbe wala hawakuwa na uhusiano wowote ule zaidi ya kufanya kazi pamoja.

Angela alipanga siku ya kumpeleka Mariamu hospitalini na jambo lile akawa anamweleza kila mtu huku shauku yake kubwa ikionekana dhahiri kuwa alitaka akathibitishe kwamba Mariamu alikuwa na ugojwa wa ukimwi. Masikini hakuna mtu yeyote aliyeonekana wala kumsaidia Mariam kwa kumpa moyo, msaada wake mkubwa ulionekana ni kutoka kwa Angela aliyeamua kumtafutia michango na kumpeleka kwa dokta. Mariam hakuthubutu kupinga chochote kile hata kama aliona hatendewi vyema kwa kuhofia kuonekana mtovu wa fadhila, ilibidi avumilie madhila yote. Kwa wakati ule ni kama vile maisha ya Mariam yalikuwa mikononi mwa Angela.

Siku mbili kabla ya siku waliyopanga kwenda kucheki afya ya Mariamu, Angela alisikika akimwambia Mariamu kwamba watakapofika kwa daktari, moja kwa moja amueleze kwamba amefika pale kupima VVU na hata kama ataogopa kumweleza dokta hivyo, basi jukumu hilo atalifanya yeye mwenyewe Angela kwa kumfahamisha kuwa Mariamu alikuwa mdogo wake wa kuzaliwa tumbo moja hivyo kafika pale ili pamoja na magojwa mengine apimwe kwanza ukimwi.

Kwa kweli sakata lile toka linaanza mpaka siku hizo mbili kabla Mariamu hajapelekwa kwa dokta kwenda kupimwa ukimwi na Angela nilikuwa naliona. Kwa bahati nzuri rafiki wa kiume wa Angela tulikuwa tunafahamiana na mara kadhaa hata mimi huwa nilikuwa nikipenda kumtania juu ya kukonda kwa “shemeji yetu Mariamu” .

Siku hiyo nilikaa naye mahali tukajadiliana “serious” kuhusu hali ya Mariamu na jinsi mwenzake Angela alivyokuwa akiichukulia hali ile ijapokuwa alikuwa akijidai kuwa anamsaidia.

“Ni msaada wa namna gani huo anaompa?” nilimuuliza boyfriend huyo wa Mariam. “Kila binadamu anahitaji uhuru wa kujiamulia mambo yake mwenyewe anavyotaka yawe, faragha na heshima hata ikiwa yupo mahututi” nilimueleza kwa uchungu. Baada ya kujadili, nikamtaka amwambie Mariam kwamba nilitaka kuzungumza naye kabla hajapelekwa hospitali siku ya Jumatatu. Mariamu siku ileile alinitafuta tukaketi mahali, na sikuchelewa, kwanza nikamuuliza “kwani wewe Angela mna uhusiano gani?” “Hatuna uhusiano wowote zaidi ya kufanya kazi naye hapa kwa bosi wetu” Alinijibu Mariamu kwa hali ya unyonge.

Niliendelea kumwambia Mariamu kwamba, hata ingelikuwa Angela ni mama yake mzazi, bado hakuwa na haki wala ruksa ya kumlazimisha eti aende kupima afya yake ili kujua hali yake ya VVU. Isitoshe nilimwambia Angela hata kama angetoa yeye mwenyewe zile pesa za matibabu, bado hakuwa na haki wala uhalali wa kumtangaza kila mahali kwa namna alivyofanya.

Nilichomshauri Mariamu ni kwamba, akubali waende haspitalini, ila wakiwa kwa dokta akatae katakata kupimwa ukimwi mbele ya Angela na aseme kama ni ukimwi basi ataamua mwenyewe kwa ridhaa yake siku nyingine wala siyo kwa kulazimishwa na mtu yeyote yule.

Kweli Mariamu alifanya vilevile kama nilivyomshauri kwa kumuumbua Angela mbele ya daktari. Daktari naye palepale alimpa Angela elimu ya kutosha juu ya haki za msingi za binadamu hususani kuhusiana na kujua hali ya kiafya ya mtu kama vvu. Mariamu alipata ujasiri wa ajabu baada ya tukio lile, na akaapa kuwa hatakubali tena siku nyingine maisha yake yawe mikononi mwa mtu wingine.

Ilikuja kubainika kumbe Mariamu alikuwa na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na wala siyo ukimwi kama wengi walivyomdhania, akatumia dawa kwa usahihi na sasa maisha yake yanaendelea vizuri.

Mfano wa pili, unamhusu mtu mmoja ambaye jina lake halisi sitaweza kulitaja, bali nitamuita tu kwa utani “Mangi”. Mangi baada ya kumaliza masomo yake na hatimaye kuanza kazi za ufundi umeme jijini Dar es salaam, aliamua kuoa na akampata mchumba kutoka mkoani Tanga ambaye naye alikuwa akiishi jijini Dar es salaam kwa dada yake aliyekuwa naye ameolewa.

Uamuzi wa Mangi ulikuwa ni kinyume kabisa na matarajio ya wazazi, ndugu na jamaa zake huko Moshi ambao walitaka Mangi akaoe nyumbani kwao kijijini alikozaliwa. Wazazi ndugu na jamaa hao walianza chokochoko hasa baba yake mzazi aliyediriki kusema hatampa radhi endapo ataendelea kuishi na mwanamke asiyekuwa wa kabila lake. Dada zake na hata kaka zake wote lao llikuwa moja, kuhakikisha Mangi haishi na mwanamke aliyemuoa.

Walimzushia mara mke wake alikuwa mchawi, alipochelewa kuzaa wakadai hazai na mambo chungu nzima. Kipato cha Mangi kilikuwa ni cha kawaida lakini ndugu zake walidai mwanamke huchukua fedha na mali za ndugu yao na kupeleka upande wa mwanamke kujenga nyumbani kwao na alikuwa amemfunga Mangi kwa dawa za kienyeji ili asiweze kumshitukia. Kwa ujumla Mangi aliwekewa vikwazo vya ajabu ajabu mpaka mwenyewe akaanza kujutia kumuoa yule mwanamke.

Kipindi fulani baba yake Mangi aliugua na kwa bahati mbaya akafariki dunia. Watoto wake wote walifika Moshi kumzika wakiwa wameongozana na wake au waume zao kasoro Mangi peke yake aliyekwenda peke yake kwani ndugu walishaapa kwamba ikiwa mke wake angekanyaga Moshi basi wangemkatakata kwa mapanga.

Kule Dar alikobaki mke wa Mangi, baada ya msiba wa baba mkwe wake alidhani labda mumewe angerudi baada ya mazishi, lakini hakumuona, alisubiri tanga liishe napo wala hakusikia simu yake. Akaamua kumpigia Mangi namba yake nayo ilikuwa haipatikani. Kimya kiliendelea mke wa Mangi na mwanaye mchanga Rafaeli wakiwa peke yao, mwezi, miezi na hata mwaka ukakatika bila hata ya kujua kama Mangi alikuwa hai au alikuwa amekufa. Hata baada ya kuwauliza baadhi ya watu waliomfahamu walimueleza tu kwa kifupi kuwa Mangi alikuwa ameshaoa mwanamke mwingine huko kwao Moshi na ndugu zake wenye uwezo wa pesa walikuwa wameshamjengea kila kitu, nyumba ya kuishi pamoja na kumfungulia biashara ya kuuza nguo za mitumba katika soko la Kiboriloni.

Mke wa Mangi aliishi kwa uchungu muda mrefu akimkumbuka mumewe bila matumaini yeyote tena ya kuja kuonana naye. Hatimaye alimpata mtu mwingine wakaanza tena upya maisha. Siku moja akiwa nje ya nyumba yao maeneo ya Kimara Baruti, alimuona Mangi akija ‘amechooka’, akashtuka sana, “Baba Rafaeli ni nini ulichosahau kwetu?”


Mangi huku machozi yakimlengalenga, alianza kumsimulia mkewe wa zamani madhila aliyokumbana nayo baada ya kwenda kuoa kwao, alimsimulia jinsi mkewe mpya alivyomnyanyasa na hatimaye kwenda kuolewa na tajiri mmoja huko Himo anayemiliki vituo vya mafuta. Siyo hivyo tu alisimulia pia jinsi ndugu zake walivyomtimua kama paka katika nyumba waliyomjengea na biashara ya mitumba kufilisika. Alieleza kuwa alikuwa akiishi na kulala katika baraza za maduka ya watu huko Kiboriloni.

Mke wake wa zamani alimsikitikia na kumwambia, “Baba Rafaeli mpenzi wangu, bado moyoni mwangu nakupenda, lakini haiwezekani tena mimi kuishi na wewe, kwani tayari kuna mwenzako keshanichukua na sasa tuna watoto wawili, tena naomba usichelewe sana hapa kwani yu karibuni kurudi kazini sasa, kama ni mwanao Rafaeli, anasoma shule ya boding, labda uje siku ya wiki end, nitamwambia aje nyumbani na nitakuwa nimempa mume wangu taarifa kuwa utafika kumuona mwanao.”

Zipo sababu nyingi zinazoweza kutufanya kukosa udhibiti wa mambo au maisha yetu kwa ujumla lakini lililokuwa kubwa sana ni suala la kiuchumi. Ukishakuwa kiuchumi unamtegemea mtu mwingine tayari, “automatically” wewe maisha yako anayadhibiti yule anayekuwezesha kiuchumi. Tazama hata suala la Mariamu na Mangi hapo juu, suala la kiuchumi “PESA” limechukua nafasi kubwa sana. Sababu nyinginezo zina uzito mdogo sana.

Athari za mtu kutokuwa na udhibiti kamili wa maisha yake huweza kusababisha madhara mengi yakiwamo mtu kushindwa kujiamulia mambo anayoyapendelea mwenyewe maishani mwake, au ndoto alizokuwa nazo tangu utotoni kama vile, kujiamulia mwenza wa maisha, kujichagulia taaluma unayopenda nk. Unaweza kufikiria ni nani atakayeweza kutatua tatizo hilo kwako?

Hatua za kurudisha udhibiti wa Maisha yako mikononi mwako.
Kwa uhakika hakuna mtu yeyote zaidi yako wewe mwenyewe anayeweza kuja na kukutatulia shida hiyo ya kutokuwa na udhibiti wa maisha yako mwenyewe. Na kamwe hautaweza kubailisha hali hiyo ikiwa wewe mwenyewe hautakuwa tayari kuwajibika kikamilifu kwa vitendo vyako.

1. Yakubali kwanza matatizo yako uliyokuwa nayo, na kukubali maana yake ni kwamba matatizo hayo ni ya kwako na wala siyo ya mtu mwingine. Kama kwa mfano ni matatizo ya kiuchumi, kubali kwanza kwamba wewe ndiye mwenye hayo matatizo. Umiliki maana yake ni udhibiti na kitu kama unakithibititi maana yake pia unao uwezo wa kubadilisha hali au mambo.

2. Anza kufanya maamuzi. 
Baada ya kubaini tatizo ulilokuwa nalo na namna ulivyokuwa tegemezi, ni wakati sasa wa kufanya maamuzi ni eneo gani katika maisha yako unalotaka kubadilisha, kama kwa mfano ni suala la kiuchumi basi ni wakati wa kuamua ni nini utakachofanya, labda ni biashara, kazi au uwekezaji wowote ule utakaokuwezesha hatimaye kuwa imara na kuacha kuwa tegemezi.


Pengine kuna vitu vinakunyima raha kwa mfano kazi uliyokuwa nayo, biashara, mahusiano nk. hufurahishwi navyo, basi ni wakati wa kuamua uachane navyo au uendelee navyo lakini huku ukitafuta njia za kurekebisha hali inayokunyima raha.

3. Fanya utafiti.
Badala ya kufanya maamuzi ilimradi tu umeyafanya, hakikisha maamuzi yako yanazingatia zile taarifa bora kabisa ulizokuwa nazo kuhusiana na ufumbuzi wa tatizo unaloamua kulitatua. Kama ni biashara basi hakikisha unazama katika biashara ile unayojua utamudu kuifanya na nyenzo za kuifanya utakuwa nazo. Kwa mfano njia Mangia liyotumia kutatua tatizo lake haikuwa sahihi, ilikuwa ni njia ya mkato iliyomsababishia kilio na kusaga meno badala ya suluhisho.

4. Vitendo, tekeleza, Maamuzi peke yake na utafiti pasipokuwa na vitendo halisi hakutoshi kuleta mabadiliko, fahamu malengo yako na uweke mikakati ya kuyafikia, hakikisha pia malengo hayo ni ya kwako mwenyewe hujashinikizwa na mtu mwingine kuyafanya.

Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio ya mtu na udhibiti wa maisha yake au uhuru aliokuwa nao wa kujiamulia mambo yake menyewe bila ya kupangiwa na mtu mwingine. Ndiyo maana hata katika nchi zile zenye maendeleo makubwa katika ujasiriamali kama Marekani na Ufaransa neno “UHURU” lina maana kubwa sana. Mjasiriamali anayebanwabanwa iwe ni na serikali, mtu binafsi ama taasisi nyingine yeyote ile hawezi kufanya jambo lolote lile la maana.

Tuchukulie mfano unamiliki bishara lakini biashara hiyo kuna mambo ambayo ni lazima watu wengine waamue kabla wewe hujayatekeleza, bila shaka biashara hiyo itakusumbua na hautaweza kuifanya kwa ufanisi unaotakiwa. Mathalani katika biashara yako unatumia umeme na mwenye nyumba ndiye anayedhibiti mita ya umeme, mwenye nyumba anaweza muda wowote kuzima umeme akidai umeisha na wewe huna namna nyingine bali kutoa pesa hata kama kweli umeme haukuwa umekwisha.

Mifano ya ukosefu wa udhibiti katika eneo hili la biashara ipo mingi na ni sababu kubwa ya wajasiriamali wengi kukwama na kutokufikia mafanikio wanayostahili katika maisha yao na dawa yake pekee ni kuamua hata kama ni kwa uchungu kiasi gani kujiondoa katika udhibiti wa namna hiyo, ni bora mtu ukaanza upya kitu kingine hata kama ikiwa ni kidogo kiasi gani kwani kitaendelea kama hakuna tena udhibiti wa mtu mwingine. Kuna watu waliachana na ubia wa biashara na kwenda kuanzisha biashara zao wenyewe japo kwa watu wa nje ilionekana ubia ule ulikuwa unawanufaisha.
………………………………………………………………………


Ndugu Msomaji wa Blogu hii, tumerudi tena katika ile kampeni yetu ya KUJIRUDISHIA UKUU WAKO ULIOPOTEA, kampeni tuliyoanza nayo mwezi ule wa kwanza mwa 2017 ulipokuwa unaanza. Katika awamu hii ya pili na ya mwisho tutahakikisha kila mtu anayefuatilia kampeni hii basi anatimiza ndoto yake ambayo ni kujirudishia tena uwezo wake aliokuwa nao hapo awali, iwe ni katika Nyanja yeyote ile mfano, kichumi, kiafya, kimahusiano nk. Na kwa wale ambao basi ndio wapo katika ubora wao watapata njia sahihi za kuhakikisha wanadumu katika ubora huo bila ya kuupoteza kwa kipindi kirefu. Fuatana nasi kila siku katika makala zetu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, blogu na kwa njia ya email yako.

Kwa vitabu  bora kabisa vya Ujasiriamali katika lugha adhimu ya kiswahili, chagua hapa katika duka la self help books, SMART BOOKS TANZANIA.  Ukihitaji kitabu chochote kile iwe ni softcopy au hardcopy wasiliana nasi kupitia namba za simu 0712202244  au  0765553030

Kupata kitabu chenye kanuni maalumu ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio katika lugha ya kiswahili bure kabisa bila malipo, bonyeza maandishi yafuatayo, KANUNI NA SIRI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO.

0 Response to "HIVI UNAJUA NI NANI ANAYEDHIBITI MAISHA YAKO?"

Post a Comment