NJIA 7 HALALI NA NZURI ZA KUPATA MAFANIKIO & UTAJIRI WA HARAKA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA 7 HALALI NA NZURI ZA KUPATA MAFANIKIO & UTAJIRI WA HARAKA

Duniani kote na hata hapa Tanzania kumejaa hadidhi na masimulizi mengi kuhusiana na utajiri na mafanikio hasa hasa suala la jinsi mtu anavyoweza akapata utajiri haraka kwa njia nyepesi zisizochosha wala kuchukua miaka mingi. Wapo wanaoamini kwamba njia hizo za kutengeneza utajiri na mafanikio haraka zipo na vile vile wapo watu wanaoamini utajiri wa haraka haupo labda uupate kupitia bahati na sibu au kutoka kwa ndugu yako wa karibu aliyekurithisha baada ya kufariki dunia.

Kiukweli mtu yeyote anaweza akawa tajiri kwa njia halali ingawa siyo kwa haraka na rahisi kama watu wengi wavyowaza, vinginevyo basi iwe tu ni kwa njia zilizotajwa hapo juu za bahati na sibu, urithi, au kwa njia haramu kama vile za wizi na ufisadi. Kuna watu wengine hufikia hata hatua za kufanya vitendo vya ajabu na vya kikatili kabisa wakisaka utajiri wa haraka ambao mwishowe huwa hawaupati au huishia jela na kupata laana na majuto maisha yao yote badala ya maisha mazuri na mafanikio waliyokuwa wakiyatamani.

Vitendo kama kuua watu kutokana na imani za kishirikina, ubakaji na hata kuamini vitu vya ajabuajabu kunakohamasishwa na waganga uchwara wa kienyeji au watu wa imani za baadhi ya madhehebu na imani zisizokuwa na msingi wowote ule ndivyo kwa kiasi kikubwa vinavyowapotosha watu kuamini kwamba kuna njia za haraka za kupata utajiri na mafanikio kipesa.

SOMA: Siri 10 alizotumia Aliko Dangote kutajirika.

Vile vile wapo watu ambao wao kwa kutaka kupata utajiri wa haraka pasipo kutoa jasho, huwapotosha watu wengine kupitia vyombo mbalimbali vya habari na hususani intaneti kwa kuwahadaa kuwa wanazo mbinu au njia za kuwatajirisha upesi, hivyo sharti lao kubwa huwa ni kulipia mafunzo, vitabu, DVD  au semina. Sisemi hamna vitu vya namna hiyo vya ukweli hapana, ila nasema katika wote wanaojinadi hivyo pia na wajanja wamo humohumo, ni kama ilivyo kwa kundi la mamba, kenge nao hawakosekani.

Kwenye hii mitandao wapo watu wengi wanaotoa mafunzo ya ukweli na yenye tija na hata ikiwa mtu unatoa pesa yako baada ya kupata huduma au bidhaa kama ni kitabu, dvd au semina, unatamka; “Kweli pesa yangu haijakwenda bure, imetoka kihalali”. Hali kadhalika wapo watoa mafunzo ambao lengo lao ni kupata pesa ‘kupitia mgongo wa kukutajirisha wewe’ Hivyo, chukua tahadhari na uwe makini vya kutosha!

Sasa basi baada ya maelezo hayo mafupi, hebu twende moja kwa moja tukazione hizo njia 7 halali kabisa na za uhakika unazoweza ukazitumia kutajirika.

1. Fungua biashara.
Kufungua biashara isijekuwa ni kufungua biashara tu hivihivi kulikozoeleka kila siku, ni lazima hapa uwe “mjasiriamali” kidogo, nikimaanisha uweke ubunifu na jitihada za kutosha. Katika ubunifu na jitihada hizo, hakikisha mambo yafuatayo unayazingatia kikamilifu;

·       Hakikisha unafanya kile kitu unachokipenda, biashara ikusisimue kuifanya na siyo uifanye basi tu ilimradi kwa kuwa inabidi uifanye.

·       Weka Mipango: Usidanganyike kuwa eti, kufanya mpango au mchanganuo wa biashara ni kupoteza muda bure. Hakuna jambo lolote duniani hufanywa pasipo kuwepo mpango, tazama harusi(vikao kila wiki), ujenzi wa majengo(ramani kwanza kabla ya jengo lenyewe), uendeshaji wa serikali(kila mwaka wabunge hukaa Dodoma kupanga) na hata pale nyumbani kwako kila siku mnapoamka asubuhi, baba na mama hukaa na kupanga siku hiyo itaendaje huku mama akiorodhesha kwenye karatasi vitu anavyopanga kwenda kununua sokoni mchana. Huo ndio mpango wenyewe! Na biashara ni hivyohivyo. 

    Tatizo watu wengi tunakuwa wavivu, huwa tunapanga vichwani basi na kuishia hapohapo. Unapoandika katika karatasi hata kama ikiwa ni kurasa1 au 2, ni bora zaidi kuliko kuuacha mpango wako kichwani, wewe ni binadamu unaweza ukasahau badhi ya vitu vya msingi mbele ya safari.

·       Juhudi zako zote ni lazima zilenge kwenye mahitaji ya wateja wako.
·       Jitangaze wewe na biashara yako, usione aibu kuwaambia wateja; “Jamani siku hizi natengeneza sabuni laini nzuri za unga, maji na za miche, njooni mnunue” au “Nimeanzisha darasa la tuisheni la chekechea pale nyumbani, waleteni wanenu jioni”

·       Ichukulie biashara yako kwa umakini na weledi wa hali ya juu na siyo kuidharau, ukiidharau na wateja watafanya hivyohivyo.

·       Wape wateja huduma za kipekee, kila mmoja ajisikie unamjali tofauti na mwingine.

·       Tumia fursa ya teknolojia za kisasa kama mitandao ya kijamii kujitangaza na biashara yako zaidi kwa wateja.

·       La mwisho lakini lenye umuhimu pengine kushinda mengine yote niliyoyataja hapa ni; “USISAHAU KUWA NA NIDHAMU YA PESA”. Pesa itoke tu pale penye ulazima. Acha wakuite, “wewe ni bahili”, “Hutoi shilingi yako”, “Sijui wewe ni ‘mchagga’ pesa ikidondoka ukiwa ‘theater’ mahututi unazinduka” lakini wewe kaza uzi tu, ipo siku utakuja kuwapa msaada mkubwa hata zaidi ya huo wanaoutaka sasa kutoka kwako.

2. Wekeza katika biashara ya majengo na ardhi(Real Estate)
Niliwahi kuandika kuhusiana na biashara hii kwenye kitabu nilichoandika cha, “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA”, nikaelezea vizuri sana jinsi biashara hii ilivyokuwa na uwezo wa ajabu wa kumtajirisha mtu katika kipindi kifupi. Kwa mfano, badala ya kukopa fedha benki au kokote kule na kuanza kuumiza kichwa jinsi ya kupata pesa(faida) au utazizalishazalisha vipi, unaweza ukaziingiza pesa hizo kwenye biashara hii na ukapunguza kwa kiasi kikubwa hatari na “stress” zitokanazo na biashara za kawaida.

SOMA: Usilaumu tena mikopo ya benki na taasisi za fedha.

Tuseme pengine mkononi unazo shilingi milioni zako mbili 2, (huu ni mfano lakini) Unakwenda benki unakopa shilingi milioni saba 7, jumla zinakuwa milioni 9. Unanunua kiwanja nje kidogo ya mji na kisha baada ya miaka labda tuseme miwili au hata mwaka huo huo ulionunua unamtafuta mtu mwingine anayekihitaji unamuuzia kwa shilingi milioni 12. Hapo tayari utakuwa umeweka kibindoni milioni tatu 3 za chapchap pasipo hata kuumiza kichwa chako wala kugombana na wateja.

Shughuli hiyo unaweza hata ukaifanya kuwa ndiyo kazi yako ya kudumu huku pengine ‘wife’ kama unaye akiendelea kuuza genge lenu au biashara nyingine yeyote ndogondogo mliyonayo kwa ajili ya kuingiza senti kidogo za kununulia vitafunio asubuhi.

Au njia nyingine unaweza ukafanya hivi; Ikiwa unamiliki nyumba yenye vyumba vya kutosha, pangisha wapangaji na hata ikibidi kama nyumba ipo eneo zuri la bashara, hama wewe na familia yako mkapange nyumba eneo nafuu huko nje kidogo ya mji. Wapangaji watawaingizia kipato cha uhakika. Kumbuka kipato cha namna hii wewe mwenyewe hauhitaji uwe pale muda wote ukisimamia ndipo kipato kiingie hapana, siyo kama ilivyokuwa kwa ajira na biashara nyingine za kawaida.

6. Fungua biashara kwenye mtandao wa Intaneti
Kuna njia nyingi unazoweza ukazitumia kuingiza pesa mtandaoni, nimezizungumzia na kuziainisha pia katika kitabu changu hicho cha; ‘Mifereji 7 ya Pesa’. Mfano mmoja, unaweza ukatengeneza video na ukairusha You tube. Kila wanapoitazama watu 1000, unalipwa dola $2.

SOMA: Hatua 7 za kuanzisha biahsra yako ndogo ukiwa kwenye ajira.

Sasa tuseme video yako ni ya kipekee kiasi kwamba baada ya kuiweka tu pale, video imesambaa haraka kama moto wa nyika, kwa maana nyingine huita; “Viral video”. Unaweza ukatengeneza mamilioni kwa muda mfupi sana mtandaoni achilia mbali njia nyinginezo kama vile, matangazo ya ‘google(Adsense)’, kuuza bidhaa na huduma mbalimbali kwenye mtandao nk.

7. Tunga kitabu, muziki au filamu.(Kutumia mawazo yako mwenyewe kuanzisha mradi wa kiuchumi)
Kama ni hadithi, basi hadithi yako uitunge kwa namna ambayo utamfanya msomaji abakie na shauku/hamu kubwa muda wote ya kutaka kufahamu tukio linalofuata litakuwaje. Muziki nao ni hivyo hivyo, muangalie kwa mfano mwanamuziki nguli Diamond Platnumz(Naseeb Abdul), tangu atoe kibao cha ‘Mbagala’, watu kila kukicha hasahasa wale mashabiki zake wanakuwa na shauku ya kutaka kujua Diamond kibao kitakachofuata kitakuwa vipi. Na kwa mtindo kama huo mtu unaweza ukatajirika hata chini ya miaka mitatu 3

Wakati natunga kitabu; Mifereji 7 ya pesa, ndani ya akili yangu njia hii kati ya zote nilizoorodhesha hapa ya kuanzisha mradi wa kiuchumi ukitumia mawazo yako mwenyewe, ndiyo njia iliyokuwa imetawala zaidi akilini mwangu hata kikawa ndicho kipengele nilichoanza nacho Sura ya Kwanza ya kitabu.

HITIMISHO.

Kutajirika kunahitaji mtu ujitume na siyo kazi ya siku moja. Ukikutana na mtu yeyote yule anayekuahidi  atakupatia njia rahisi zitakazo kuwezesha kupata utajiri haraka kwa siku moja, mwezi au hata miezi kadhaa tu, mtu huyo mtilie mashaka. Huenda wewe ukawa ndiye unayekwenda kumtajirisha yeye. Badala ya kuhangaika usiku na mchana ukisaka njia nyepesi za kupata utajiri, muda huo utumie kikamilifu kujiongezea maarifa zaidi ya biashara(kunoa ubongo wako) na huku ukiendelea kufanya kazi au biashara yako kwa nguvu zako zote na maarifa, utajiri utaupata tu.

Ndugu msomaji wa makala hii, ukipenda kuwasiliana na nasi kwa ajili ya jambo lolote lile, iwe ni ushauri juu ya biashara, au ungehitaji vitabu vyetu, basi namba za simu ni hizi hapa chini;

Simu:            07122 202244 au 0765 553030 au 0689303098
E-mail:          jifunzeujasiriamali@gmail.com
Telegram:     @petertarimo

Usisahau pia kudownload hapa kile kitabu cha kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio kwani muda wake wa kutolewa bure karibu utamalizika na kitakuwa kikiuzwa kwa Sh. 5,000/=. Vitabu vingine vilivyopo katika duka letu la mtandaoni, SMARTBOOKSTZ navyo vyote sasa unaweza kuvipata kupitia simu yako ya Smartphone au kompyuta ya kawaida kupitia e-mail na telegramu. 
           

7 Responses to "NJIA 7 HALALI NA NZURI ZA KUPATA MAFANIKIO & UTAJIRI WA HARAKA "

  1. Naam Nimefurai kupata maelezo yenu ya njia bora za kibiashara itakayo wezesha mtu kujikimu kimaisha nakuweza kutoka katika hali flani ya maisha na kwa nyingine na huu ndo uhalisi wa mambo, ila swali langu ni,..wasiokua ata na uwezo wa pesa taslim zakujifungulia biashara awa nao watatumia njia gani ?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante sana Mr. Abu Muhammad kwa kusoma hapa, ni kweli kabisa shida kubwa inayowakabili watu wengi wanaotaka kujikwamua katika hali ngumu ya maisha ni ukosefu wa kianzio kwa maana ya mtaji hasa wa pesa.

      Kiuhalisia hakuna biashara isiyohitaji mtaji japo kinadharia husemekana kwamba unaweza kuanza na mawazo yako tu. Ndiyo kuna walio na bahati ya kuanza na mawazo kisha wakapata sapport mahali pengine na wakainuka lakini kwa waliokuwa wengi utakubaliana nami kwamba wanazeeka na mawazo yao kichwani.

      Lakini hata hivyo suluhisho lake lipo japo siyo njia ya mkato, kwa mfano huna pesa kabisa lakini una nguvu zako na afya uliyojaliwa na Mungu basi tafuta angalao kibarua au kazi ya ajira, utafanya kwa muda fulani huku ukijiwekea akiba kwa ajili ya kupata kianzio cha biashara unayoipenda au ikiwa una mali(asset) yeyote ile hata kwa mfano simu yako ya mkononi unaweza ukaiweka rehani mahali au kuiuza pesa zile ukaanzishia mradi wa biashara ndogo.

      Katika hatua za awali tukubaliane utapata hali ngumu sana lakini ukiwa na malengo na uvumilivu itafika tu mahali utakuwa na mtaji wa kutosha na hatimaye sasa utaweza kujitanua zaidi kwa kwenda taasisi za fedha wakuongezee mtaji wako.

      Delete
  2. ninafurahishwa sana na makala haya ya ujasiriamali yananitia nguvu na mwamko

    ReplyDelete
  3. makala haya yananipa kiburi cha kukomaa ktk ujasilamali

    ReplyDelete
    Replies
    1. Vizuri Veronica umesema kweli kwani ujasiriamali unahitaji mtu kuwa king'ang'anizi mpaka unafikia malengo yako. Waliofanikiwa wote wamefanya hivyo na wala hakuna njia ya mkato.

      Delete
  4. Thanks never give up

    ReplyDelete