MAPENZI NA MJUKUU WA UMRI WA MIAKA 9 YAMHAMISHA BABU WA MIAKA 70 MTAA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAPENZI NA MJUKUU WA UMRI WA MIAKA 9 YAMHAMISHA BABU WA MIAKA 70 MTAA


Ama kweli ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni. Ukisoma kichwa cha habai hii hapo juu, moja kwa moja utasema sasa hawa jamaa wanakoelekea siko tena kama wameanza kuandika stori za udaku badala ya zile za ujasiriamali na biashara walizozizoea. Lakini sikuwa na namna nyingine ya kuzielezea hisia zangu kuhusiana na kile nilichokishuhudia mimi mwenyewe na macho yangu leo alfajiri. Na kumbuka humu katika hii blogu kuna “segment”(kipengele) kinachohusiana na watoto na ni wajibu wangu pale ninapopata wazo linalohusiana na watoto basi niliandikie.

Tetesi za babu huyu kuanza kumnyemelea kimapenzi mtoto wa miaka tisa anayeishi na mama mmoja tuliyekuwa naye jirani, zilianza tangia mwezi ule wa June mwaka huu baada ya mama huyo kubaini bintiye huyo anayemsaidia kazi za nyumbani alikuwa anapata pesa ambazo alikuwa haelewi anayempatia ni nani.

Msichana huyo alichukuliwa na huyo mama kutoka Mkoani Mtwara alikokuwa akiishi na mama yake mzazi katika mazingira magumu kwa makubaliano kwamba aje amsaidi kazi ndogondogo za nyumbani kipindi mama huyo akiwa mjamzito na kisha mwakani angalao amtafutie shule aanze masomo. Kwa upande wake naye Babu anayehusishwa na kadhia hii, ni mwangalizi wa chumba cha kijana mmoja anayemwita mwanaye(siyo wa kumzaa lakini) huyo kijana bada ya kupanga chumba hicho huwa hakai humo mara kwa mara kutokana na shughuli zake kuwa ni za ujenzi wa nyumba, hivyo kulazimika muda mwingi kulala ‘site’ nje ya mji au hata wakati mwingine kusafiri kwenda kujenga huko Mikoani. Babu ni baba mdogo wa huyo kijana na wanao ndugu zao wengine, dada zake na huyo kijana ambao wala hawaishi mbali sana na alipopanga huyu kijana yaani eneo mkasa huu ulipotokea.

Babu huyo nyakati za mchana huwa mara nyingi anashinda kwa hao wanawe wa kike ambao nao wala sio wakwake wa kuwazaa bali ni watoto wa mdogo wake. Kisha muda wa jioni ndipo babu hurudu kuja kulala kwenye chumba cha huyo kijana. Leo sasa mbele ya mjumbe wa nyumba kumi na majirani kibao waliofika kuja kushuhudia babu huyo akihamishwa, mtoto yule wa kike ndipo alipoambiwa aeleze jinsi yeye na babu walivyoanza uhusiano wao, akaanza kusimulia kuwa mara ya kwanza kabisa babu alimkuta akitokea bombani ndipo akamuuliza, “wewe huyu mama unayekaa naye unamuitaje?” binti akasema alimjibu, “mimi nafanya kazi kwake” babu akamwambia tena, “basi mimi siku moja nitakuchukua tuende kwetu Tanga ukatembee”.

Binti aliendelea kusimulia kwamba, babu mara kwa mara huvizia watu wote nyumbani anakokaa binti na hata baadhi ya wale majirani wa karibu wanapokuwa wameshaondoka kwenda makazini basi yeye humpelekea zawadi za aina mbalimbali yakiwemo mayai ya kuchemshwa, karanga na fedha.

Mwezi ule wa sita baada ya mama huyo kubaini mwenendo wa mashaka wa msichana na binti huyo, aliwaita kina mama wote majirani wapatao kama sita hivi na kuwaeleza lakini kina mama hao wengi wao walikataa kata kata kuamini kama babu yule kweli angeliweza kufanya vitendo vya namna ile. Waliomtonya huyo mama juu ya uhusiano huo haramu walikuwa ni watoto wake mwenyewe mama wa miaka mine na sita wanaoshinda na huyo binti mchana kuwa babu mchana wakati watu wazima hawapo babu huwa anamletea dada yao mayai ya kuchemsha, karanga na pesa.

Basi kina mama wale wote kwa pamoja walikubaliana kumlinda binti huyu mdogo kwa kila mmoja kuhakikisha pindi anapobakia nyumbani basi ahakikishe anafuatilia nyendo za Yule babu kuona kama ataendelea kumfuatilia tena yule binti ama la. Binti naye kwa upande wake alipewa onyo kali na wale kina mama kuwa asimsogelee kabisa yule babu na hata akimpelekea zawadi yeyote basi aikatae na kumuita mtu mzima yeyote aliekuwa jirani amueleze.

Kina mama wale hawakuishia tu pale, wakamuita mjumbe pamoja na yule babu mtuhumiwa wakamkalisha kikao na kumueleza yote japo yule babu alipinga na kukataa kata kata kuhusika, alidai ni kawaida yake kuwapa watoto wote zawadi ndogondogo kama hizo na wala habagui wakati anapowagawia.

Miezi ya hapo katikati mmoja wa wale kina mama aliwaeleza wenzake kwamba ana wasiwasi yule babu atakuwa bado hajaacha tabia zake kwa kuna mwanaye mdogo wa miaka 5 alimwambia kuna siku moja babu alimuita yule binti akampa shilingi 500 pamoja na kumshikashika(Leo wakati binti akisimuli, alidai babu amewahi kumshikashika sehemu  za siri ila hakufanya naye kitendo kibaya)

Mama mlezi wa huyu binti liwaambia kinamama wenzake kuwa suala lile asingeliweza kulifikisha mbali zaidi kama polisi  mpaka kwanza apate ushahidi wa kutosha kwahiyo kinamama wakakaa tena kikao kingine cha kuzidi kupanga mikakati ya kumlinda yule binti ikiwa ni pamoja na kutafuta ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka.

Binti kuna kipindi alichukuliwa na kupelekwa kwa mama mmoja ndugu na mama mlezi wa huyo binti kwa lengo la kukaa kule wiki moja kusudi achunguzwe vizuri juu ya vitendo vilivyokuwa vikiendelea baina ya yule binti na babu. Ripoti ya yule mama ikaonyesha kuwa babu alikuwa bado akimfuatilia yule binti na alikuwa amekwishampatia zawadi chungu nzima pamoja na kumshikashika mara kadhaa sehemu zake za siri pamoja na kifuani. Ila kwa bahati nzuri binti alipoulizwa iwapo babu alimuingilia kimwili alisema hakuwahi kufanya hivyo ila alikuwa mara kwa mara akimshawishi aingie chumbani kwake yeye akawa anakataa.

Yote hayo tisa, kumi ilikuwa ni jana siku ya Alhamisi mchana. Mmoja wa wale kina mama majirani hakuwa amekwenda kwenye mihangaiko yake, muda kama saa saba hivi za mchana akiwa umbali kidogo akamuona binti akizungumza na yule babu wakiwa kandokando ya bonde la mto unaokatiza jirani na nyumba anayokaa binti. Yule mama alijibanza nyuma ya ukuta wa nyumba huku akiendelea kuwatazama kama kingeendelea kitu gani.

Wakati huohuo kumbe kuna vijana wawili nao wenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 18 na 20 waliokuwa wamekaa kwenye uwanja wa kuchezea mpira ulioko jirani. Kwa kuwa na wao walishakuwa na taarifa za skendo hiyo, vijana hao nao walikuwa wakifuatilia mchezo wote ili, babu akizama tu kule bondeni na yule binti basi na wao waende wakammalizie kulekule.

Yule mama hakuweza kuendelea kuangalia, ikambidi asogee karibu na kule yule binti na babu walikokuwa. Binti akajifanya anaondoka zake huku yule babu akijidai kumuuliza yule mama kwa butwaa, “ Hivi huku kuna njia ya kutokea kule ngambo ya mto?” Mama naye akamjibu kwa kebehi, “Hakuna njia kwani wewe ulijua utatokajetokaje huku”

Kimbembe sasa ikawa ni jioni. Mama mlezi aliporudi kutoka mihangaikoni kwake akapokelewa na yule binti mwenyewe akimueleza kuwa leo babu alimfuata tena akitaka kumpa pesa. Kumbe binti baada ya kugundua yule mama keshawaona na kwa vyovyote vile ni lazima angekuja kumueleza jirani yake atakaporudi, basi akaamua mwenyewe kumshitaki kabisa babu mapema kabla hata ya mama yule kwani alishaonywa akimuongelesha tu atoe taarifa.

Mama wa ajirani alipojua tu jirani yake karudi, alimuita na kumsimulia kisa chote kilivyokuwa mwanzo mpaka mwisho. Wale vijana wa kiume nao mmoja kati yao alikuwa akizungumza na mama yake jioni hiyo akimsimulia kisa cha binti mchana. Mama yake na kijana alikuwa mmoja kati ya wale kinamama huyo naye ni miongoni mwa wale kina mama majirani walioazimia kumlinda yule binti.

Mwishowe jioni hiyohiyo kinamama wotw wale majirani walikutana tena na kuambiana; “Jamani sasa tumekwisha pata ushahidi wa kutosha, babu ni lazima aende jela” Wakaenda kwa mjumbe usiku ule ule na kila kitu wakawa wamekwisha kukiweka sawia.

Alfajiri ya leo yapata kama saa kumi na moja hivi, nikasikia kishindo nje, ni mjumbe alikuwa akigonga mlango wa kile chumba cha yule babu. Bahati kijana mwenye chumba chake naye alikuwepo, jana hakulala ‘site’. Kijana ndiye wa kwanza kutoka, akahamaki, kwanza hata mjumbe mwenyewe kijana huyo hawakuwa wanafahamiana. Kijana akawa anafoka, “Ni ustaarabu gani huo kutugongea mlango usiku usiku tena utafikiri sisi ni wahalifu, kwanini usije taratibu tu, hata raisi hawezi akagonga hivyo” Kijana hakuwa anafahamu chochote juu ya sakata lile. Mjumbe naye alikuwa na hasira, akamwambia, “Kwanza tunamhitaji sasa hivi huyo sijui ni babu yako sijui ni baba mimi sielewi, yuko wapi”

Wakati yote hayo yakiendelea, eneo zima lilikuwa limeshajaa kina mama na mwanamume pekee aliyekuwepo pale ni mjumbe na mume wa yule mama mlalamikaji basi. Baadaye kidogo na mimi nilitoka ndani nilikokuwa nimelala nikajisogeza pale karibu. Baadaye kidogo kijana alielezwa kisa chote tangu kilivyoanza na walishindwa kumpa taarifa kutokana na yeye kutopatikana mara kwa mara. Kwa kweli kijana hakuamini kabisa masikio yake kwamba baba yake mkubwa yale ndiyo mambo aliyokuwa akiyafanya. Alipiga simu kwa dada zake na kwakuwa hawaishi mbali sana na pale eneo tukio lilipotokea nao wakawasili haraka. Baada ya kuelezwa nao waliangua kilio utadhani wamefiwa.

Hata hivyo huyo dada mkubwa alikuwa tayari amekwisha elezwa kisa hicho na mama mmoja naye akamwambia baba yao ni kweli tabia zake siyo za kuridhisha sana na inavyoonekana ni kama vile ameathirika kisaikolojia kwani alifiwa na mke wake siku nyingi na isitoshe hajawahi kuwa na mtoto hata mmoja wa kumzaa mwenyewe. Inasemekana pia babu huyu enzi zake alikuwa ni mtu wa kujirusha maklabu na sehemu za starehe sana.

Wanawe kilichowaliza zaidi si kingine, bali ni kufikiria jinsi ambavyo baba yao mkubwa atakavyokwenda kuanza upya maisha ya jela wakati afya yake wanaijua wenyewe ilivyo. Ilibidi pale busara zaidi zitumike kwani baada ya pale babu ilikuwa apelekwe moja kwa moja kituo cha polisi kufunguliwa mashitaka ya ubakaji mtoto mdogo. Wanawe walikiri kweli kuwa baba yao mkubwa hakuwa na sababu ya kuja kugawa zawadi kwa watoto wa mbali wakati anao wajukuu zake(watoto wa hao mabinti zake) na hata siku moja hajawahi kuonekana akiwanunulia, pipi za big bom, karanga na mayai kama alivyokuwa akifanya kwa yule binti. Babu kujitetea alijiumauma akidai kuwa yeye hakuwa na nia yeyote mbaya kwa yule binti.

Wengine walimshauri yule mama amrudishe yule binti huko kwao Mtwara lakini wengine wakapinga na kudai kwamba, hata kama atarudishwa bado hiyo siyo dawa kwani pale mtaani bado kuna watoto wadogo wa kike wengi, hivyo babu inawezekana akaja akaendelea na azma yake hiyo ya kutaka kuwaharibu na pengine huwezi hata kujua labda anayo maradhi yake anayoamini kwa, kuviambukiza vibinti vichanga basi yeye anaweza akapata ahueni.

Kina mama wote wale hawakukubali kirahisi kumuacha hivihivi yule babu ingawa wanaye walimuombea sana msamaha. Wakafikia uamuzi wa pamoja kuwa, huruma wanayompa yule babu na ni kwa kuwa alikuwa hajatimiza bado azma yake hiyo ovu ni ama ahame kabisa pale mtaani au vinginevyo kesi isonge mbele wao wapo tayari kwenda kusimama naye kizimbani na kwa kuwa tayari ushahidi wanao wakutosha ni lazima wahakikishe wanamfunga.

Babu hakuwa na jinsi, zaidi ya kukubali kufungasha virago na wanawe kwanza walifurahi mno kuona kuwa sasa baba yao mkubwa hapelekwi tena polisi. Kulikuwa sasa kumeshaanza kupambazuka, babu aalipotaka akapige mswaki mjumbe akamwambia, “Babu unapoteza muda, chukua kilichokuwa chako hautakiwi tena hapa mtaani kwangu”. Babu akajitetea ataondoka Jumatatu lakini wale kinamama katu wakakataa asiendelee kuonekana tena pale vinginevyo basi mjumbe atomize wajibu wake wa kumfikisha kituo cha polisi.

Wanawe walimsaidia babu kutoa nje kila kilichokuwa chake wakamsaidia kubeba na kuondoka naye, huku babu akitamka maneno, “Mmenionea tu bure, Mungu mwenyewe ndiye anayejua”

Kisa hiki nimelazimika kukiweka hapa kwasababu nimekishuhudia mwenyewe kwa macho yangu. Na huyo babu kusema ukweli, angelikuwa anasikia ya watu, wala aibu yote hii isingempata ikiwa ni pamoja na kunusurika tundu la sindano kwenda jela. Aliwanunia kina mama wote pale jirani kisa eti ni wambea wanamfuatilia maisha yake wakati mama mwenyewe mlezi wa yule binti wala hakuwa na neno.

Kumbe babu hakuwa anafahamu kuwa kinamama wale pamoja na mlalamikaji wote lao lilikuwa moja na walikuwa wakimuonya kumkinga yeye na mabaya na wakati huo huo wakimlinda yule binti mdogo asije akaharibiwa ndoto zake angali bado mchanga kiasi kile. Walivuta subira wapate ushahidi na hakuna kitu kizuri katika kesi yeyote ile kama ushahidi na ushahidi ndio hasa uliokuja kumuumbua huyu babu.

…………………………………………………………………………
Mlinde mtoto popote pale ulipo,
Kwani na wewe pia kuna wakati ulikuwa mtoto,
Leo kafanyiwa wa mwenzako,
Na kesho ni zamu ya wakwako au wa ndugu yako.       

0 Response to "MAPENZI NA MJUKUU WA UMRI WA MIAKA 9 YAMHAMISHA BABU WA MIAKA 70 MTAA"

Post a Comment