MAISHA YA MAFANIKIO?: SOMA VITABU HIVI VYA BIASHARA NA UJASIRIAMALI KWA KISWAHILI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAISHA YA MAFANIKIO?: SOMA VITABU HIVI VYA BIASHARA NA UJASIRIAMALI KWA KISWAHILI

Katika makala zetu siku za nyuma niliwahi kuandika makala iitwayo, NI KITABU GANI HAUTAKISAHAU MAISHANI?. Kitabu ambacho mimi siwezi kukisahau maishani, siyo lazima wewe ama  mtu mwingine naye iwe hivyo hivyo, kila mtu anaweza akawa na mtizamo wake tofauti kuelekea kitabu/vitabu fulani.

Tanzania na Duniani kwa ujumla wake, vimewahi kuandikwa vitabu vingi vya kila aina, kuanzia vile vya Dini, elimu na maarifa mbalimbali mpaka vile vya hadithi na riwaya. Kuna vitabu vikubwa na vidogo vilivyoandikwa katika lugha mbalimbali kutoka katika mabara yote ya dunia kuanzia Asia, Ulaya Amerika, Afrika na Australia.

Vitabu ndiyo chimbuko la Ustaarabu duniani kote, kwa mfano inasemekana maandishi ya kwanza kabisa yalianza kutumiwa huko Sumeria ya kale katika karne ya 3 -7 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo (IRAQ YA LEO) kati kati ya mito ya Tigris na Euphrates katika mfumo uliojulikana kamapictographic’ au maandishi yanayowakilisha picha za vitu halisi badala ya herufi kama hizi tunazotumia leo hii.

Mpaka kufikia maendeleo ya sasa ukiachilia mbali teknolojia ya kompyuta na mtandao wa intaneti vilivyoibuka hivi karibuni tu, ni vitabu na maandishi ya aina mbalimbali yaliyokuwa yakitumiwa katika kurithisha maarifa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine ijapokuwa pia katika jamii nyingine ambazo hazikuwa na maendeleo makubwa kiteknolojia mfano maeneo mengi ya Afrika, Australia na hata  Amerika walikuwa wakitumia njia za masimulizi kueneza na kurithishana maarifa kutoka kizazi hata kizazi.

Katika tasnia ya biashara na Ujasiriamali hapa Afrika ya mashariki na hususani nchini Tanzania, vipo vitabu vingi tu vinavyohusiana na taaluma hizo lakini kwa bahati mbaya sana vingi vimeandikwa katika lugha ya kiingereza, na utakuta mara nyingi mtu anapotaka kusoma kitabu fulani basi ni sharti awe na kamusi(dictionary) pembeni kwa ajili ya kutafsiri(translate english to Swahili).

Tatizo hili la lugha ya kiingereza kwa hapa Afrika ya Mashariki lipo kwa sisi Watanzania zaidi kuliko nchi zingine kama Kenya na Uganda, na hii imetokana hasa na mfumo wetu wa Elimu tangu enzi zile za Mwalimu ambapo tumekuwa “Mshika mawili”, kiswahili tunataka na kiingereza nacho tunakitaka kwa wakati mmoja, mwishowe tunajikuta kila moja hamna tunayoimudu barabara. Huwezi ukamkuta mtu Kenya au Uganda akisoma kitabu cha kiingereza na huku pembeni eti kaweka na kamusi ya kiswahili.

Kwa kweli ili maarifa ya aina yeyote yale mtu aweze akayapata yakamwingia vizuri zaidi kichwani na hatimaye akawa na uwezo wa kuyatafsiri kivitendo(translation of knowledge into action) kwa urahisi pasipo kuhangaika na kamusi wala ‘google translator’, basi hana budi kuijua bara bara lugha anayoitumia kujifunzia.

Vitabu vingi vizuri vya Biashara, Ujasiriamali na maendeleo binafsi, siyo siri, vimeandikwa katika lugha ya kiingereza. Sina maana kuwa hamna vya kiswahili vilivyokuwa vizuri, la hasha, vipo ingawa siyo vingi kama ilivyokuwa vya kiingereza.

Ikiwa uwezo wako katika lugha ya kiingereza ni mzuri kwa kweli hauna shida ya kusoma vitabu vizuri, vipo vingi sana hata nikisema nivitaje hapa patakuwa hapatoshi. Tukianza na kitabu maarufu zaidi duniani cha pesa na mafanikio “THINK & GROW RICH” au kwa ‘jina la utani’ “MSAHAFU WA MAFANIKIO”, kitabu hiki kinapatikana bure kabisa mtandaoni pasipo kulipa hata senti hamsini,download kitabu hicho hapa free, ukitaka katika lugha ya kiingereza au katika mitandao mingine kinapopatikana.

Lakini tukirudi  katika mada yetu kuu iliyokuwa ikisema, “Kwa maisha ya mafanikio: Soma vitabu hivi vya Biashara na Ujasiriamali kwa Kiswahili”, bila shaka ndugu msomaji utakuwa na shauku ya kutaka kuvijua hivyo vitabu ni vipi, na mimi sikukudanganya kwani dhima yangu kuu ni kuhakikisha kila ninachokiandika humu kwenye blogu ni sahihi na kimefanyiwa utafiti wa kutosha kabisa.

Umuhimu wa kusoma au kujifunza maarifa iwe ni ya kisayansi, ya kibiashara, ya kihandisi, ya kitabibu, ya kiufundi au ya aina nyingine yeyote ile katika “LUGHA YAKO YA MAMA” nikiwa namaanisha ile lugha yako uliyojifunza toka utotoni ni mkubwa sana kwani humsaidia mhusika kuelewa haraka na kwa urahisi zaidi tofauti na kutumia lugha ya pili au ya tatu. Kuna mifano mingi kwa mfano Wachina, Wajerumani, Wakorea, Wajapani, Wavietnam na hata Warusi, huzitumia lugha zao za mama kujifunza maarifa ya aina zote kuanzia fasihi, sayansi na teknolojia, biashara, ufundi mpaka aina zote za ufundi na uhandisi. Na wanafanikiwa kufanya vizuri hata kuwashinda waanzilishi wenyewe wa teknolojia hizo Waingereza na Wamarekani.

Kitabu cha “Think & Grow Rich” licha ya kuwa unaweza ukakisoma kwa lugha ya  kiingereza pia unaweza ukakisoma katika lugha ya Kiswahili fasaha kabisa bila ya kuwa na kamusi  pembeni ya kiingereza-kiswahili(English to Swahili) kupitia blogu hii ya jifunzeujasiriamali. Kitabu hiki kitakufunulia siri nyingi na mbinu mbalimbali matajiri wengi na watu mbalimbali waliwahi kufanikiwa kimaisha, njia walizopitia mpaka kufikia pale walipofikia.

Vitabu vingine vya Ujasiriamali, Biashara, Pesa na Mafanikio katika lugha adhimu ya Kiswahili pia unaweza ukavipata kutoka kampuni ya Self Help Books PublishersLimited. Vitabu kama vile, “Jifunze Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali”, “Siri ya Mafanikio ya Biashara ya Rejareja” na “Mifereji ya Pesa na Siri Matajiri wasiyopenda kuitoa”. Mbali na vitabu vya Self Help Books, pia kuna waandishi wengine wengi tu wa Kitanzania, vitabu vyao vimeandikwa kwa Kiswahili na unaweza ukavipitia ikiwa vitakupendeza. Tuachane na ile kasumba mbaya ya kudharau kila kinachofanywa na Watanzania wenzetu. Mfano mmoja ni mtu mmoja tena mwandishi mwenzangu aliyenishangaza sana kwa kudiriki kuandika katika blogu yake kuwa yeye hasomi tu hovyo hovyo vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa hapa nchini.

Akataja baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa ngambo akidai ndivyo yeye hupenda kuvisoma. Kwa maoni yangu huyu hawezi kuwa mwandishi mzuri kwani mwandishi unapaswa usome kazi za watu wengine hata ikiwa unaamini kiwango chao ni kidogo ndipo utaweza kujua wewe unao uwezo gani. Kumbuka ile kanuni maarufu ya soko isemayo, “Katu usiwadharau washindani wako”

Narudia tena kusema kuwa, kama wewe upo vizuri katika lugha ya kiingereza, una uwezo wa kuitumia pasipokuwa na vipingamizi vinngi ikiwa ni pamoja na uwezo hata wa kufikiri kwa kutumia lugha hiyo, siyo kusoma tu na kuandika pekee, basi unaweza ukajisomea vitabu vilivyoandikwa katika lugha hiyo na vikakupa manufaa yaliyokusudiwa bila ya kutumia nguvu nyingi na muda. Ushauri wangu ni kwamba ukitaka kujifunza kitu kwa urahisi na haraka zaidi basi tumia ile lugha unayoielewa vizuri zaidi na mara nyingi huwa ni ile lugha ya mama uliyoanza kujifunza muda mfupi baada ya kuzaliwa kwani ndiyo ubongo wako uliyoizoea zaidi.

Njia mbadala, unaweza ukaamua basi ikiwa kile unachotaka kujifunza kipo katika lugha fulani tofauti na ile lugha yako ya mama madhalani katika kiingereza, basi suluhisho ni wewe kuhakikisha unajifunza vyema na kukizoea kiingereza ili wakati wa kukitumia basi usipate vikwazo.


0 Response to "MAISHA YA MAFANIKIO?: SOMA VITABU HIVI VYA BIASHARA NA UJASIRIAMALI KWA KISWAHILI"

Post a Comment